Monday, February 20, 2012

NILIZALIWA N IWE MBUNIFU WA MITINDO - "MANJU MSITA

Mbunifu wa Mitindo,Manju Msita,akiwa kazini kwake.
Ni siku ya Jumamosi,nipo jijini Dar-es-salaam tayari kabisa kwenda kuonana na miongoni mwa wabunifu wa mitindo (Fashion Designer) mahiri kabisa hapa nchini, Manju Msita. Tofauti na siku zingine za Jumamosi,leo hakuna msongamano mkali wa magari barabarani.Hii si kawaida sana kwani siku hizi jiji la Dar-es-salaam lina sifa mbaya ya kuwa na foleni zisizokwisha.
Kwa muda nimekuwa nikiwasiliana na Manju.Hatujawahi kuonana.Sina hata hakika kama yeye ameshawahi kuona picha yangu.Mimi nishawahi kuona yake kutokana na ukweli kwamba Manju ni mbunifu maarufu,sio tu nchini Tanzania bali katika ukanda mkubwa wa Afrika.
Ofisi au karakana(workshop) ya Manju ambapo ndipo yalipo makao makuu ya Smart Africa,kampuni ya masuala ya mitindo na ubunifu anayoiongoza Manju,zipo maeneo ya Chang’ombe.Zamani palikuwa na kituo kikubwa cha sanaa cha Mikono Arts.
Nawasili maeneo yale na kupokelewa vizuri na kila mtu.Manju ana timu nzuri.Wapo vijana, wa kike na kiume,wenye uchangamfu wa ajabu.Namkuta Manju ameketi huku kajiinamia.Mkononi kashikilia pencil.Mara moja nachungulia anachokifanya na kuona wazi alikuwa akichora.Anaacha anachokifanya na kusimama kunikaribisha.Manju anapenda utani.Mara moja tunaanza mazungumzo ya kawaida huku nikiwa na shauku ya kuanza kufanya kilichonipelekea(mahojiano). Anakuja dada mmoja na kwa sauti ya unyenyekevu ananiuliza kinywaji ninachotumia.Naagiza maji ili panapo kuanza kwa mazungumzo,koo lisije kunikauka.Maji yanawekwa mezani,naanza kuweka koo langu sawa.
Kabla ya kuendelea mbele,Manju anaomba anipe kwanza tour ya ofisi yake na kunitambulisha kwa watu wake.Kila kona ya ofisi yake imepambwa kwa nakshi za kiafrika au zenye utambulisho wa kiafrika.Natizama michoro ya magauni,nageukia kule na kuona magauni,mashati nk.Haya naambiwa mengine yanauzwa na mengine yanasubiri wenyewe kuja kuchukuliwa.
Tunarejea ofisini kwake.Hapo nagundua kwamba kuna mziki laini unaimba.Muziki wa kiafrika.Nasikia sauti ya Habib Koite.Kisha namsikia Oliver Mtukudzi.Tunaendelea kusikia muziki kwa mbali na mazungumzo yetu yanaanza kama ifuatavyo;
BC: Unakumbuka ulianza lini safari yako ya kuwa mbunifu wa mitindo?Nini au nani alikuvutia kuingia katika fani hii?Ni mambo gani ya msingi ambayo ilikubidi ujifunze mara moja pindi ulipofanya uamuzi wa kuwa mbunifu wa mitindo?



MM: Safari hii sikuianza kwa kubahatisha,kwa vyovyote nilizaliwa ili iwe hivyo.Niliianza pale nilipokuwa tumboni kwa mama huku mwalimu akiwa ni Mwenyezi Mungu mwenyewe.Nadhani siku niliyozaliwa ndiyo nilitunukiwa shahada ya ubunifu kwa vile hajatokea wala hatatokea Mwalimu wa kunifundisha kubuni labda wa kunielekeza jinsi ya kuutumia vyema ubunifu huu. Ikumbukwe ya kwamba kubuni ni kufanya kile ambacho hakijawahi kuwepo zaidi ya hapo ni kuiga. Huwezi kubuni kile ambacho tayari umekiona bali utaiga.

Aliyenivutia kuingia kwenye fani hii ni Mungu mwenyewe baada ya kunifundisha nikiwa tumboni na kunikabidhi shahada siku niliyozaliwa.

Nilipoamua kuingia kwenye fani (kimatendo) kwa kweli sikuwa na mengi sana ya kujifunza zaidi ya kubuni na kuwaachia mafundi washone.Mama yangu ni mwalimu mstaafu wa maarifa ya nyumbani (Domestic Science) na katika kukua kwangu nimejifunza mengi toka kwake mojawapo likiwa ni hili.


BC: Mpaka hivi leo umeshiriki katika maonyesho mangapi ya ubunifu wa mitindo na ni yepi ambayo unaweza kusema hutokaa uyasahau daima?Kwanini?


MM: Mpaka sasa nimeshashiriki maonyesho yapatayo kumi na nne ndani na nje ya nchi na mengi mengine yanakuja. Maonyesho yote hayo yamekuwa changamoto kwangu kwa vile unakutana na akili tofauti zifanyazo ubunifu tofauti.
HII HAPA CHINI NI SLIDESHOW INAYOONYESHA UBUNIFU WA MANJU MSITA.UKITAKA KUIONA PICHA IN FULL KWA UKUBWA,BONYEZA JUU YAKE
 
Manju Msita'S Designs

BC: Baadhi wa wabunifu wa mitindo ambao nimewahi kuzungumza nao iwe katika mahojiano maalumu au hata katika mazungumzo ya kawaida tu wanasema sio lazima kwa mbunifu wa mitindo kwenda shule na kusomea chochote katika fani hii.Yaani mtu anaweza kuamka tu asubuhi akasema anataka kuwa mbunifu wa mitindo na akaanza kufanya hivyo.Una maoni gani kuhusu dhana  au mtazamo kama huo?


MM: Si kweli kwamba unaweza ukaamka asubuhi na kuamua kuwa mbunifu wa mitindo,hiki si kikombe cha chai kwamba kila mtu anaweza kunywea…ni suala la kutumia maarifa zaidi kuliko elimu au utundu.
Wagunduzi wengi wakubwa duniani walitumia maarifa zaidi kuliko elimu,maarifa kwa maana ya kuzaliwa nayo na si kufundishwa. Aliyegundua ndege alitumia maarifa bali anaesomea uhandisi au urubani leo hii anatumia elimu.Huwezi ukakurupuka na kuamua kuwa mbunifu,mbunifu wa kweli hutenda kweli…


BC: Tangu nimeingia hapa ofisini kwako nimegundua kwamba …wewe ni mchoraji mzuri na kwamba ubunifu wa mitindo yako unaanzia kwenye michoro.Unadhani kujua kuchora kuna umuhimu gani katika fani nzima ya ubunifu wa mitindo kwani nimeshawahi kukutana na Fashion Designers ambao hawajui kabisa kuchora!


MM: Mimi ni mchoraji wa kuzaliwa na ndio maana katika maisha yangu imekuwa rahisi kwangu kufanya graphic designing/cartoons/paintings na vinginevyo.Unaponiona ninachora sio kwamba ninabunini kwamba nilishabuni na sasa ninachora.Wapo wabunifu wengi wazuri na wakubwa duniani ambao si wachoraji. Kwa kuwa wana ubunifu vichwani mwao,wanachotakiwa ni kuelekeza wachoraji au washonaji…nadhani hata wao wanatamani wangekuwa wachoraji kwakuwa ingewarahisishia sana kazi.


BC: Ni ushauri gani wa msingi ambao ungempa mtu anayetaka kuingia katika fani ya ubunifu wa mitindo hivi leo hapa Tanzania kwa mfano?


MM: Kama ni mbunifu wa kweli basi na atumie uwezo wake wote bila kukata tamaa huku akiweka nia nafsini mwake kwamba amezaliwa ili ashinde. Akili yako inapokwambia huwezi basi kufanikiwa kwako ni ndoto.


BC: Ubunifu wa mitindo unakwenda sambamba na kitu ambacho wenzetu wanakiita “inspiration”.Kwa upande wako unapata wapi “inspiration’ zako au yako?


MM: Napata ‘inspiration’ kutokana na mazingira yanayonizunguka ‘nature’.Naweza kupata idea toka kwa wanyama,ndege,samaki,nyumba,majani,milima na vingine vingi.


BC: Ipo dhana kwamba kila kitu kinachotoka magharibi (everything from west) au nchi za Ulaya na Marekani ni bora kuliko vya kwetu.Unazungumziaje dhana kama hii na unadhani inaathiri kwa kiasi gani soko la wabunifu wa mitindo kama wewe hapa nchini Tanzania?


MM: Ni kweli vipo vingi toka magharibi ambavyo ni bora ila si kweli kwamba vyetu havifai. Ndani ya bara la Afrika kuna ubunifu wa hali ya juu sana nadhani tunachohitaji kufanya ni kuongeza ubora wa bidhaa zetu(quality),kupunguza gharama za uzalishaji ili mnunuzi amudu bei, kujiamini na kufanya kazi kwa bidii zetu zote pia tuache kuwaza na tuanze kufikiri.

Ni wazi kwamba kiasi kikubwa dhana hii inaathiri soko la wabunifu wetu.Kwa mfano mtu anasema yeye ni mbunifu lakini anachokifanya ni kilekile kinachofanyika Ulaya na Marekani ila pengine anatumia kanga/kitengeau kuchukua hiki na kile toka huko na kuviunganisha pamoja.Huku ni kudumaza ubunifu na kukomaza uigaji matokeo yake ni kukosa ‘identity’. Nadhani ni wazo zuri kuendeleza kilicho chako ndani ya nchi yako.


BC: Bila shaka yapo mambo mengi sana ambayo umeshajifunza tokea uingie katika fani ya ubunifu wa mitindo.Je,ni mambo gani ambayo unadhani ungeyajua kabla hujaingia katika fani hii pengine yangebadilisha kabisa mtazamo wako katika fani hii?


MM: Ndani ya fani ubunifu wa mitindo nimeshajifunza mengi kwa mfano kutokata tamaa,umuhimu wa kutumia akili za ziada na kwamba maendeleo ya mwanadamu hayatokani na rangi yake au vinginevyo bali ni maamuzi yaliyo kichwani mwake yaliyo katika mpangilio na mwelekeo ulio sahihi.


BC: Ni jambo au mambo gani ambayo ungependa watu wayaelewe kuhusu fani ya ubunifu wa mitindo ambayo unahisi hayaeleweki hususani miongoni mwa watu ambao sio wabunifu wa mitindo?


MM: Ubunifu si rahisi kama wengi wanavyodhani,ninapopita kwenye mitaa ya Dar es salaam huwa naona sehemu mbalimbali za ushonaji zikiwa zimeandikwa ‘……fashion designer’.lakini kinachofanyika pale si ubunifu bali ni uigaji.

Kwa bahati mbaya wengi hudhani hata kuiga ni kubuni. Jambo lingine ambalo halifahamiki vizuri ni ile hali ya kudhani nguo ya kununua dukani ni ghali zaidi kuliko unayoshonewa.Pengine hii inachangiwa na kiwango duni cha nguo unayoshonewa kuliko unayonunua dukani na hii ni changamoto kwetu ili tuongeze viwango vya ubora unaoenda sambamba na dunia inavyotaka.Jambo hili linawezekana kwa sababu akili ni zilezile,mashine ni zilezile labda tofauti ni mazingira.


BC: Hivi sasa unamiliki kampuni au label ya Smart Africa.Unaweza kunieleza kidogo kuhusu malengo haswa ya Smart Africa na ilikuwaje ukaamua kuanzisha Smart Africa pamoja na changamoto ulizokabiliana nazo ulipokuwa unaanzisha hii kitu?


MM: Smart Afrika ni kampuni iliyojaa ubunifu wenye mwelekeo na mtazamo wa kimataifa. Ni kampuni inayokubali kwamba dunia sasa ni kijiji na kwamba penye nia siku zote pana njia.
Wakati naanzisha kampuni hii nimekumbana na changamoto nyingi zikiwemo kutojiamini kwa mafundi (tailors),ukosefu wa baadhi ya malighafi na mashine, na kubwa zaidi ni mtaji mdogo.


BC : Hivi sasa ulimwengu mzima unapambana na kitu kinachoitwa “Uharibifu wa mazingira”.Wabunifu wengi wa mitindo wanakabiliwa na changamoto ya kuwa wa “kijani” au kwa kiingereza being Green kwa maana ya kushiriki kikamilifu katika kuhakikisha kwamba uharibifu wa mazingira unakuwa wa kiwango cha chini kabisa.Wewe kama mbunifu wa mitindo hapa Tanzania unakabiliana vipi na changamoto hii yenye sura ya ki-ulimwengu mzima?Masuala ya utunzaji mazingira unayachukuliaje?


MM : Uhifadhi wa mazingira ni jambo muhimu sana kwa kizazi kilichopo na kijacho,kwa kuzingatia hilo kampuni yetu inahakikisha hatutoi mifuko ya nailoni/plastiki kwa wateja wetu bali ya makaratasi maalum au vitambaa. Pia tupo mbioni kwa kushirikiana na kampuni nyingine itengenezayo vikoi kuanza kutengeneza nguo zitokanazo na pamba isiyo na kemikali (organic cotton) ili afya ya mvaaji isiwe hatarini.

BC : Wateja wako ni kina nani hasa ?

MM: Wateja wangu ni wale wapendao kupendeza huku wakiwa katika mwonekano tofauti kimavazi. Ni wa rika mbalimbali wanaoheshimu na kuelewa nini maana ya ubunifu.Wanatofautiana kimapato kwani wapo wamama wa nyumbani,mabalozi hadi mawaziri. Nawaheshimu sana watu hawa kwani wao pia wanatumia akili kuchagua mavazi sahihi kwao.

BC : Bila shaka kazi yako na pengine maisha yako binafsi yamekupa nafasi ya kusafiri katika nchi mbalimbali hapa ulimwenguni.Katika kutembelea nchi hizo na katika kulinganisha,kwa mfano,fani ya ubunifu wa mitindo katika nchi hizo na hapa kwetu,ni yapi ambayo umeyaona na kusema hili ni zuri na sisi pia tunaweza kuliiga na kulileta hapa nchini?Ubunifu wa mitindo…
MM : Hapa kwetu ubunifu wa mavazi bado ni fani changa sana yaani kama ni mtoto basi ndio kwanza anatambaa. Wenzetu wa ulaya, marekani na nchi zilizoendelea wameanza karne nyingi zilizopita na kwa vyovyote vile wako mbele yetu.Kuendelea kwao hakutakiwi kuwa kikwazo kwetu bali changamoto. Ubunifu tunao kwa karne nyingi zilizopita ila tatizo letu ni kutojiamini na kutoweka ubunifu wetu katika kumbukumbu pia kutoutumia katika matumizi ya kisasa yanayoendana na dunia ya leo. Mambo ambayo nimeyaona na kuyapenda toka kwao ni pamoja na;
v  ubunifu wa mavazi ni biashara inayoweza kuwa kubwa sana iwapo utaamua iwe hivyo.
v  nchi za wenzetu muda ni mali wakati sisi muda ni jua kusogea,wenzetu wawapo kazini hawatakiwi kusikiliza au kupokea simu wakati kwetu usishangae ukaitwa mnyanyasaji
pale unapomkataza mtu kufanya hivyo.
v  wakati watu duniani wanaishi kwa kutumia maarifa,sisi bado tunatumia mazingira na ndio maana miaka hamsini baada ya uhuru bado tunasubiri mvua inyeshe ili tupate umeme, ni mambo ya ajabu kabisa!
v  kwa wenzetu umaliziaji (finishing) ni muhimu sana ila kwetu bado kitabu kinauzwa kwa kuangalia jalada. Pengine hii inachangiwa nauchanga wa hii fani hapa kwetu.
v  bara la afrika lina nafasi nzuri katika soko la nguo duniani kwa vile tunao ubunifu wapekee ambao bado haujasambaa. Tunachohitajika kufanya ni ni kuuweka katika katika sura ya kidunia ili wavaaji wawe wanadunia na si waafrika pekee.

BC: Kama sikosei kazi ya ubunifu wa mitindo ni kama haina kikomo.Hata ukiwa mapumzikoni unaweza kuona kitu fulani cha ki-mtindo kikakuvutia na kukufanya uwaze na kuwazua.Pamoja na hayo bila shaka kuna wakati na wewe hupenda kupumzisha akili na roho na kuwa mbali na ulimwengu wa mitindo.Ukiwa mapumzikoni unapenda kufanya mambo gani?
MM : Bahati mbaya sina uwezo wa kuisimamisha akili iache kufikiri na macho yaache kuona. Hata niwapo mapumzikoni naweza nikaona kitu fulani na akili ikaamua kukifanyia kazi,si vibaya kwangu ila ingekuwa vyema kama ningepata muda mzuri zaidi kusikiliza muziki, kusoma habari za watu mashuhuri waliofanikiwa maishani,kujua zaidi kuhusu wabunifu mashuhuri na wakubwa duniani,kulala vizuri,kufanya mazoezi n.k.
BC: Asante sana kwa muda wako Manju.It was a pleasure
MM:Asante Jeff.Karibu tena na tena…

Read more: “NILIZALIWA NIWE MBUNIFU WA MITINDO”-MANJU MSITA - BongoCelebrity

No comments:

Post a Comment


Labels